Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania imetangaza kuzindua huduma ya Airtel 4G, ikiwa ni muendelezo wa kupanua wigo wa mtandao wake nchini.
Akizindua huduma hiyo jijini Dodoma, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji Angella Kairuki amesema kuwa, ni furaha kuona Airtel inatekeleza mipango ya uwekezaji na kuja na huduma za mtandao wa Airtel 4G, kwa lengo la kukidhi mahitaji ya Watanzania wote.
“Wote tunatambua kuwa Airtel Tanzania na Serikali yetu waliingia makubaliano mazuri hivi karibuni, makubaliano ya kwamba Serikali yetu iwe na umiliki wa asilimia 49 wa hisa ndani ya Airtel Tanzania, kutokana na makubaliano hayo pia hadi leo Airtel Tanzania imeshailipa Serikali jumla ya Shilingi Bilioni Nane kama sehemu ya makubaliano hayo na leo hii Airtel wanatekeleza upanuzi wa mtandao”, amesema Waziri Kairuki.
Pia ameipongeza Airtel kutokana na taarifa yao inayoonesha kasi ya kusambaza huduma hiyo ya Airtel 4G katika miji mikubwa takribani 25, ambapo leo wamewasha mtandao wa Airtel 4G mkoani Dodoma.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, -George Mathen amesema kuwa, uzinduzi huo wa huduma ya Airtel 4G ni moja ya malengo ya muda mrefu ya kuifanya kampuni ya Airtel kuwa na uwezo wa kutoa huduma bora.
