Serikali yakiri kuwepo kwa upungufu wa chakula kwenye baadhi ya maeneo

0
142

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa, baadhi ya maeneo nchini yana upungufu wa chakula kutokana na maeneo hayo kukumbwa na hali mbaya ya hewa ikiwa ni pamoja na ukame.

Akijibu Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu Bungeni jijini Dodoma, Waziri Mkuu Majaliwa amewaagiza viongozi wa maeneo yote yenye upungufu wa chakula nchini kuandaa taarifa kuonyesha uwepo wa tatizo hilo na kuiwasilisha Serikalini ili taratibu nyingine zifuatwe.

Katika swali lake la Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu, Mbunge wa jimbo la Chemba, -Juma Nkamia aliuliza kuwa Serikali imejipanga vipi kuwasaidia Wakazi wa maeneo mbalimbali nchini, wanaokabiliwa na upungufu wa Chakula kutokana na viongozi wa maeneo hayo kuogopa kutoa taarifa za tatizo hilo kwa kuhofia kupoteza nafasi zao.

Katika jibu lake, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa, Serikali inafahamu kuwa kuna maeneo yaliyokumbwa na hali mbaya ya hewa na kusababisha kutokuwa na chakula cha kutoka, hivyo kwa kuzingatia hilo hakuna haja kwa kiongozi yeyote kuwa na wasiwasi kuwa hajatimiza wajibu wake katika kuhimiza uzalishaji wa chakula.

Amefafanua kuwa, kosa kwa Kiongozi ni pale ambapo eneo lake linaruhusu uzalishaji wa chakula na ameshindwa kuhimiza uzalishaji huo na kusababisha upungufu wa chakula.

Waziri Mkuu Majaliwa pia ametoa wito kwa Wafanyabiashara nchini kutumia fursa hiyo ya upungufu wa chakula katika baadhi ya maeneo, kusafirisha chakula na kwenda kuuza katika maeneo hayo.