Serikali imesisitiza kuwa, kila Mtanzania atapata haki yake ya msingi ya kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, unaotarajiwa kufanyika Novemba 24 mwaka huu.
Kauli hiyo ya Serikali imetolewa Bungeni jijini Dodoma na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati wa kipindi cha maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu.
Amesema kuwa, tangu kuanza kwa mchakato huo wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa, taratibu zote zimekua zikifuatwa, hivyo hakuna haja kwa Mtanzania yeyote kuwa na wasiwasi wa kukosa haki yake ya msingi.
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania wote kujitokeza kusikiliza Sera za Wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi, pindi kampeni za uchaguzi huo wa Serikali za Mitaa zitakapoanza Novemba 17 mwaka huu na kujitokeza kuwachagua Viongozi wanaowataka itakapofika siku ya uchaguzi.
Awali Mbunge wa Iramba Mashariki, – Allan Kiula alimuuliza Waziri Mkuu Majaliwa kuwa, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha Watanzania wote wenye haki ya kupiga kura katika uchaguzi huo wanafanya hivyo, kwa kuwa kwa sasa wengi wana wasiwasi kuwa hawatapata haki ya kushiriki katika uchaguzi huo.
