Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) imeitaka Serikali ya Guinea pamoja na upande wa upinzani, kuanza tena mazungumzo yenye lengo la kutafuta amani kufuatia kuendelea kwa maandamano na mauaji nchini humo.
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, – Fatou Bensouda ameonya kuwa, watu wote wanaoendeleza machafuko na mauaji nchini Guinea wanaweza kufunguliwa mashtaka katika Mahakama za nchini humo ama ICC.
Upande wa upinzani nchini Guinea umesema kuwa, watu 16 wameuawa tangu mwezi Oktoba mwaka huu, baada ya kuanza kwa maandamano nchini humo.
Raia wa Guinea walianza maandamano baada kuwepo kwa taarifa kuwa, Rais Alpha Condé wa nchi hiyo, ana mpango wa kuifanyia mabadiliko Katiba ya nchi hiyo ili aweze kugombea kiti cha Urais kwa muhula wa Tatu.
Tayari Mahakama hiyo ya Kimataifa ya Uhalifu yenye Makao Makuu yake mjini The Hague nchini Uholanzi, imechunguza mauaji ya zaidi ya Wafuasi 150 wa Upinzani wa nchi hiyo, waliouawa mwaka 2009 katika uwanja wa Mpira uliopo kwenye mji Mkuu wa Guinea, -Conakry.