Shirikisho la Soka Ulimwenguni (FIFA) limemfungia kwa muda wa miaka Kumi kujishughulisha na masuala ya Soka Kitaifa na Kimataifa aliyewahi kuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), – Jamal Malinzi baada ya kumkuta na hatia ya matumizi mabaya ya fedha na kughushi nyaraka.
Mbali na adhabu hiyo, Malinzi pia amepigwa faini ya Dola 503,000 za Kimarekani ambazo ni zaidi ya Shilingi Bilioni 1.1 za Kitanzania.
Uamuzi huo umetolewa na Kamati ya maadili ya FIFA, baada ya kufanyika kwa uchunguzi uliobaini kuwa, Malinzi alihusika katika matumizi mabaya ya fedha za FIFA, fedha za CAF, fedha nyingine za TFF pamoja na kughushi nyaraka za maazimio ya Kamati ya Utendaji ya TFF kati ya mwaka 2013 na mwaka 2017.
Adhabu hiyo imeanza kutekelezwa Novemba Nane mwaka huu na tayari Malinzi mwenyewe amekwishajulishwa.
Taarifa iliyotolewa na FIFA hii leo kupitia mitandao mbalimbali imeeleza kuwa, Kamati hiyo ya Maadili imemkuta Malinzi na hatia ya kuvunja kanuni ya 24 inayohusu kughushi nyaraka, na kanuni ya 28 inayohusu matumizi mabaya ya fedha katika kanuni za maadili ya FIFA toleo la mwaka 2018, na hivyo kumfungia miaka kumi kujihusisha za shughuli zote za soka Kitaifa na Kimataifa