Mfumuko wa bei katika bidhaa zisizo za chakula wapungua

0
3168

Mfumuko wa bei wa Taifa kwa kipimo cha mwaka unaoishia mwezi Oktoba mwaka 2019, umeongezeka hadi asilimia 3.6 kutoka asilimia 3.4 mwaka ulioishia mwezi Septemba mwaka huu ikiwa ni ongezeko la asilimia 0.2.

Akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dodoma, Kaimu Mkurugenzi wa Takwimu za Jamii na Sensa ya Watu, – Ruth Minja amesema kuwa, ongezeko hilo limetokana na kasi ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Oktoba mwaka huu, ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba.

“Ongezeko hili la mfumuko wa bei limetokana na ongezeko la bei za bidhaa za vyakula na vinywaji baridi, ambapo mfumuko wa bei kwa mwezi Oktoba mwaka huu umeongezeka hadi asilimia 5.1 kutoka asilimia 4.0 mwezi Septemba mwaka huu wa 2019”, amesema Kaimu Mkurugenzi huyo wa Takwimu za Jamii na Sensa ya Watu.

Aidha amesema kuwa, mfumuko wa bei kwa bidhaa na huduma zote ambazo hazijumuishi chakula na nishati kwa mwezi Oktoba mwaka huu umepungua kidogo hadi asilimia 2.6, kutoka asilimia 2.7 mwezi Septemba mwaka huu.

Serikali kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ambayo ndiyo mamlaka ya kutangaza takwimu, imekuwa na utaratibu wa kutangaza matokeo ya mfumuko wa bei kila mwezi.