Madaktari JKCI wafanya upasuaji wa Kwanza wa aina yake

0
146

Kwa mara ya kwanza, Madaktari Bingwa wa upasuaji wa Moyo kwa Watoto katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es salaam, wamefanya upasuaji wa kutenganisha mshipa wa damu wa kusambaza damu kwenye mwili na kuweka mshipa bandia wa kusambaza damu kwenye mapafu.

Upasuaji huo uliochukuwa muda wa Saa Nne na Nusu, umefanyika kwa mtoto mwenye umri wa miezi Mitano ambaye alikuwa na tatizo la  damu safi na chafu kutokea  kwenye mshipa wa damu mmoja badala ya mishipa miwili tofauti.

Akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Daktari Bingwa wa upasuaji wa Moyo kwa watoto kutoka JKCI, -Godwin  Sharau amesema kuwa wameweza kutengeneza mshipa wa damu bandia ambao unabeba damu chafu kutoka kwenye chumba cha chini  cha kulia cha moyo na kupeleka kwenye mapafu ili kutenganisha damu chafu na safi.

“Katika upasuaji huo tumeweza pia kuziba tundu la moyo na kulitenganisha kutoka kulia na kushoto ili kuweza kusaidia mzunguko wa damu kuwa katika hali ya kawaida, mshipa huu bandia utadumu kwa muda wa miaka 10 hadi 15, baada ya hapo utabadilishwa  na kuwekwa mkubwa zaidi tofauti na wa sasa ambao ni mdogo, na aina hii ya magonjwa ya Moyo ni  nadra sana kutokea lakini katika mazingira yetu tumekuwa tukiwaona watoto wenye matatizo kama haya na Watoto kama hawa wasipopata matibabu ndani ya miezi sita tangu kuzaliwa kwao wanaweza kupoteza maisha”, amefafanua Dkt. Sharau.

Ameongeza kuwa, kwa mwaka huu wamefanya upasuaji wa aina hiyo kwa wagonjwa Watatu, ambapo Wawili walifanyiwa upasuaji katika kambi maalum ya matibabu ya Moyo ya Wataalam kutoka nchini Italia na Ujerumani na huyu wa sasa amefanyiwa na Madaktari wazawa wa Taasisi hiyo ya Moyo ya Jakaya Kikwete.