Wimbo wa Tarimbo wafutwa mitandaoni

0
1878

Mwenyekiti wa Bodi ya Filamu nchini Kenya (KFCB), – Dkt Ezekiel Mutua ameipongeza kampuni ya Google kwa kuuondoa kwenye mitandao ya kijamii wimbo wa Tarimbo, ulioimbwa na kundi la Ethic Entertainment la nchini humo.


Kupitia akaunti zake kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na ule wa Facebook, Dkt Mutua ameishukuru kampuni hiyo ya Google kwa kuunga mkono jitihada za Kenya za kuhakikisha maadili yanalindwa.


Kampuni ya Google imeufuta kabisa wimbo huo na kuonya kulichukulia hatua kundi hilo la Ethic, endapo litaweka tena mitandaoni nyimbo zinazofanana na hiyo.


Dkt Mutua ambaye anafahamika kwa msimamo wake mkali wa kusimamia maadili ya Kenya amesema kuwa, wimbo huo wa Tarimbo haukuzingatia maadili na haufai kabisa kwa kuwa unadhalilisha Wanawake.


Hivi karibuni, kundi hilo la Ethic liliomba radhi kutokana na wimbo huo wa Tarimbo kuwa na baadhi ya maneno ya kukera na kusisitiza kuwa kosa hilo halitajirudia tena.