Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za MItaa (TAMISEMI), – Selemani Jafo ametangaza kuwa, Wagombea wote waliochukuwa fomu na kuzirejesha wanaruhusiwa kushiriki kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 24 mwaka huu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dodoma, Waziri Jafo ametangaza kufutwa kwa maamuzi yote yaliyofanywa na Wasimamizi wa uchaguzi ya kuwaengua Wagombea wa vyama mbalimbali.
“Natoa Muongozo, Wagombea wote waliochukuwa fomu na kuzirejesha waruhusiwe kushiriki uchaguzi huo, waingie ulingoni, hakuna kutafuta sababu, labda kama sio Raia wa Tanzania, hajajiandikisha Kwenye Mtaa husika, amejiandikisha mara mbili au hajadhaminiwa na chama chake”, amefafanua Waziri Jafo.
Aidha Waziri Jafo amebainisha kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimepita bila kupingwa katika baadhi ya maeneo kwenye uchaguzi huo wa Serikali za Mitaa kutokana na kutokuwepo kwa Wagombea kutoka vyama vingine.
Amesema CCM imepita bila kupingwa katika vijiji 6,248 kati ya 12,319, mitaa 1,169 kati ya 4,263 na vitongoji 37,505 kati ya 64,384
