Miili 126 imeopolewa hadi hivi sasa kufuatia ajali ya kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere iliyotokea hapo jana Septemba 20.
Idadi hiyo imetangazwa jijini Mwanza na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe katika mahojiano yake na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
Amesema kuwa miili zaidi imepatikana kufuatia kazi ya uokoaji inayoendelea hivi sasa katika eneo kilipozama kivuko hicho.
Mhandisi Kamwelwe amesema kuwa taarifa kamili ya serikali itatolewa baadae hii leo kama zoezi la uokoaji litaendelea hadi kesho ama litasitishwa hii leo.
Kwa mujibu wa Waziri Kamwelwe, hadi sasa miili 31 imekwishatambuliwa.
Kivuko cha MV Nyerere kinachotoa huduma zake kati ya Bugorora na Ukara wilayani Ukerewe mkoani Mwanza kilizama wakati kikiwa katika safari zake za kawaida.