Afrika yatakiwa kutotegemea misaada kutoka nchi tajiri

0
211

Rais John Magufuli amewataka Viongozi wa Bara la Afrika kubadili fikra na mtazamo wa kutegemea misaada na utegemezi wa kiuchumi kutoka nchi tajiri, na badala yake kutumia Diplomasia ya uchumi kuwa msingi wa ushirikiano katika kuleta maendeleo ya haraka kwa Wananchi wake.

Akizungumza jijini Dar es salaam katika ufunguzi wa mkutano wa 18 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za NORDIC na Bara la Afrika, Rais Magufuli amesema kuwa uhuru wa kisiasa uliozipata nchi za Bara la Afrika hautakuwa na maana iwapo nchi zake zitaendelea kutegemea misaada kutoka nchi tajiri.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, Bara la Afrika lina mambo mengi mazuri yanayoweza kulisaidia katika kujikwamua kiuchumi kupitia ushirikiano wake na nchi za NORDIC ikiwa ni pamoja na fursa za biashara na Uwekezaji.

“Ushirkiano wetu na Nchi za NORDIC ni wa miaka mingi, na tumekua tukitegemea misaada kutoka nchi hizo, Viongozi wa Afrika tunapaswa kutambua kuwa mustakabali wa Mataifa yetu upo mikononi mwetu, ni lazima tuondokane na aina hii ya ushirikiano”, amesisitiza Rais Magufuli.

Aidha amesema kuwa, Bara la Afrika lina utajiri mkubwa wa raslimali na vivutio mbalimbali vya biashara na uwekezaji ukilinganisha na Nchi za NORDIC, lakini hata hivyo Mataifa hayo ya NORDIC yamekuwa yakipiga hatua kubwa za maendeleo ya kiuchumi ikilinganisha na Nchi za Bara hilo la Afrika.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, – Profesa Palamagamba Kabudi amesema kuwa , kwa miaka mingi nchi za NORDIC zimekuwa rafiki wa kweli kwa Bara Afrika ikiwemo Tanzania, ambapo tangu uhuru wa Tanzania nchi hizo zimekuwa zikisaidia ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway, -Ine Eriksen Soreide amesema kuwa, nchi za NORDIC zitaendelea kushirkiana na Mataifa ya Bara la Afrika katika kuleta maendeleo ya Wananchi wa Bara hilo.