Waliodhulumu fedha za Wakulima wa ufuta wakamatwa

0
142

Zaidi ya Viongozi 300 kutoka Vyama 31 Vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) mkoani Lindi, wamekamatwa kwa tuhuma za kudhulumu fedha za Wakulima wa zao la Ufuta.

Kukamatwa kwa Viongozi hao kunafuatia agizo la Rais John Magufuli alilolitoa Oktoba 15 mwaka huu, akiwa katika ziara yake wilayani Ruangwa mkoani Lindi baada ya kupatiwa taarifa kuwa Wakulima wa Ufuta wilayani humo wamedhulumiwa fedha zao.

Katika agizo lake, Rais Magufuli aliitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchiji (TAKUKURU), kuhakikisha wanawakamata na kuwachunguza Viongozi wote wanaotuhumiwa na fedha hizo zirejeshwe kwa Wakulima.

Akizungumza na Waandishi wa Habari wilayani Liwale mkoani Lindi, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Brigedia Jenerali John Mbungo amesema kuwa, mbali na kuwakamata  Viongozi hao, pia Taasisi hiyo imeokoa zaidi ya Shilingi Milioni 630.

Aidha TAKUKURU imekamata mali mbalimbali za Viongozi hao wa AMCOS pamoja Wafanyabiashara walioshirikiana nao katika kuwadhulumu Wakulima fedha zao.

Brigedia Jenerali Mbungo ameongeza kuwa, operesheni ya kuvichunguza Vyama Vya Ushirika ni la nchi nzima na  tayari wameanza kuvichunguza vya mikoa ya Simiyu Mwanza, Arusha na Tabora .