Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekatisha ziara yake mkoani Dodoma na kuelekea wilayani Ukerewe mkoani Mwanza kuwafariji wananchi waliopatwa na maafa kufuatia kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere.
Waziri Mkuu Majaliwa ambaye alikuwa na ziara ya kikazi ya siku saba mkoani Dodoma ametangaza uamuzi huo wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Chandama wilayani Chemba ambao walisimamisha msafara wake ili wamueleze kero kubwa ya maji inayowakabili.
Waziri Mkuu alikuwa akitokea kijiji cha Itolwa kata ya Jangalo ambako alikuwa na mkutano wa hadhara na kuwaeleza wakazi wa vijiji vya Itolwa, Mapango na Chandama kuwa serikali imetenga shilingi bilioni tano nukta sita kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maji kwenye wilaya hiyo.