Serikali imeongeza bajeti kwa ajili ya kununua Dawa na Vifaa Tiba kutoka Shilingi Bilioni 31 mwaka 2015 hadi kufikia Shilingi Bilioni 270 mwaka huu.
Akitoa tathmini ya utendaji kazi wa Serikali ya awamu ya Tano katika kipindi cha miaka Minne, Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt Hassan Abbasi amesema kuwa, bajeti hiyo ya kununua Dawa pamoja na Vifaa Tiba imeongezwa ili kuziwezesha Hospitali na vituo vya afya vinavyoendelea kujengwa nchini kutoa huduma bora za afya pindi vinapokamilika.
Kwa mujibu wa Dkt Abbasi, zaidi ya Watumishi Elfu Sita wa sekta ya Afya wameajiriwa, ikiwa ni sehemu ya kuboresha huduma katika afya nchini.
Ameongeza kuwa Serikali imejenga Hospitali mpya 68 za wilaya katika maeneo mbalimbali nchini ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, lengo likiwa ni kusogeza huduma karibu zaidi na Wananchi.