Serikali kutoa Shilingi Bilioni 40 kesho kulipa Wakulima wa Korosho

0
258

Rais John Magufuli ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kutoa Shilingi Bilioni Arobaini kwa ajili ya kumalizia madeni yote ya wakulima wa korosho yaliyobaki, baada ya Serikali kununua korosho za Wakulima katika msimu wa mwaka 2018/2019.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo Ikulu jijini Dar es salaam, alipokutana na viongozi wa Wizara mbalimbali, Mikoa, Wilaya na Taasisi za Serikali ambazo zinahusika katika uzalishaji na mauzo ya zao la Korosho.

Pamoja na kuiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kutoa fedha hizo hapo kesho, Rais Magufuli pia amewaagiza viongozi wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha fedha hizo zinawafikia Wakulima na sio vinginevyo, na kuhakikisha wanalipwa Wakulima wanaostahili.

Rais Magufuli ameelezea kutoridhishwa na utendaji kazi wa Wizara ya Kilimo pamoja na viongozi wa Mikoa na Wilaya ambao katika maeneo yao kumetokea wizi mkubwa wa fedha za Wakulima kupitia vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS), hali iliyosababisha Wakulima wengi kuishi maisha duni.

Amesema amesikitishwa kuona viongozi wa Wizara, Mikoa na Wilaya hawajachukua hatua madhubuti dhidi ya watu wanaowaibia Wakulima mpaka alipoamua kumtuma Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) Brigedia Jenerali John Mbungo ambaye kwa muda mfupi amebaini kuwepo wizi wa Shilingi Bilioni 1.23 na tayari amefanikisha kurejeshwa kwa Shilingi Milioni 375 katika Mkoa wa Lindi pekee.

Rais Magufuli amewataka viongozi wa Wizara ya Kilimo, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kubadilika na kuhakikisha haki za Wakulima zinalindwa ipasavyo kwa kurejesha fedha zilizoibwa na kuzuia mianya yote ya wizi.

“Nataka mfanye kazi, hakuna mtu wa kuwanyanyasa, nendeni mkashughulikie kero za Wakulima, mna vyombo vya ulinzi na usalama nendeni mkavisimamie, kinyume na hapo nitakuona hutoshi kwenye nafasi hiyo”, amesema Rais Magufuli.

Kuhusu minada ya korosho, Rais Magufuli ametaka utaratibu uliowekwa wa kufungua mnada kuanzia saa Mbili asubuhi hadi saa Kumi Jioni na kisha kufungua masanduku yenye zabuni kwa uwazi mara baada ya saa Kumi jioni uheshimiwe, ili kuepusha njama za upangaji wa bei.

Viongozi wa Mikoa na Wilaya waliokutana na Rais Magufuli hii leo, wamemuahidi kwenda kusimamia maelekezo yake na kuhakikisha haki za Wakulima zinalindwa.

Mkutano huo wa Rais Magufuli na viongozi wa Wizara mbalimbali, Mikoa, Wilaya na Taasisi za Serikali ambazo zinahusika katika uzalishaji na mauzo ya zao la Korosho pia umehudhuriwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.