AfDB yaongezewa mtaji

0
4551

Mkutano maalum wa Tano wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kauli moja umekubali na kuridhia ongezeko la mtaji wa Benki hiyo kutoka Dola Bilioni 90 za Kimarekani hadi Dola Bilioni 283.
 
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mkutano huo huko Abidjan nchini Ivory Coast, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi amesema kuwa, uamuzi wa mkutano huo ni wa kihistoria.
 
Amesema kuwa, uamuzi huo unaifanya Benki ya Maendeleo ya Afrika kuwa na uwezo mkubwa wa kufadhili miradi mbalimbali na mikubwa ya kimkakati katika Bara la Afrika, na hivyo kuliwezesha Bara hilo kupiga hatua kimaendeleo 
 
Profesa Kabudi amezitaja faida ambazo nchi za Afrika zitazipata kutokana na kuongezeka kwa mtaji wa Benki hiyo ya Maendeleo ya Afrika kuwa ni pamoja na kuwa na uwezo wa kutoa mikopo mikubwa na ufadhili kwa ajili ya kutekeleza miradi mikubwa na ya kimkakati.
 
Kwa upande wake Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Dkt Yamungu Kayandabila amesema kuwa, kutokana na Bara la Afrika kuwa na nchi nyingi masikini, uwepo wa Benki ya Maendeleo ya Afrika unatoa ahueni kwa nchi hizo na kutoa wito pia kwa Taasisi binafsi kutoka nchi za Kiafrika kuchangamkia fursa ya ongezeko la mtaji wa Benki hiyo.
 
Benki ya Maendeleo ya Afrika ambayo illianzishwa kwa lengo la kuchochea maendeleo ya Bara hilo, inamilikiwa kwa asilimia Sitini na nchi za Kiafrika na asilimia nyingine Arobaini zinamilikiwa na nchi waalikwa kutoka katika mabara mengine Duniani.