Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, – Simon Sirro amekemea tabia ya baadhi ya watu wanaomiliki silaha za moto, kutishia kwa kuwapiga risasi watu wengine, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
IGP Sirro ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam, baada ya kuzindua rasmi kampeni ya UTATU ambayo ni kwa ajili ya kupambana na vitendo vya rushwa barabarani.
Amesema kuwa, watu wamemilikishwa silaha si kwa ajili ya kutishia watu wengine, hivyo wanapaswa kutozitumia vibaya na kwamba watu wanaokiuka taratibu za matumizi ya silaha hizo hatua kali lazima zichukuliwe.
IGP Sirro amelazimika kutoa kauli hiyo kufuatia kusambaa picha katika mitandao mbalimbali ya kijamii, ikimuonyesha mtu mmoja anayemtishia mwenzake kwa silaha katika mazingira ambayo hayakuwa yanasababu kwa mmiliki wa silaha hiyo kuitumia.
Amesema kuwa, Jeshi la Polisi nchini linaendelea kumtafuta mtu huyo aliyetishia kwa silaha, na silaha hiyo anatakiwa kunyang’anywa kutokana na kuitumia vibaya.
“Watu wanatumia silaha visivyo, sasa Jeshi la Polisi linamtafuta mtu huyo na popote akikamatwa sheria itashika mkondo wake kwa kutumia silaha vibaya kwa kutishia Wananchi”, amesema IGP Sirro.
Ameongeza kuwa, silaha hizo zimekuwa zikiombwa kwa sababu ambazo wanaamini ni kwa matumizi sahihi na salama, lakini kwa makosa yanayopatikana kwa baadhi ya watu wanaokiuka taratibu za matumizi ya silaha hizo, hatua