Ujenzi wa Meli mpya na Chelezo washika kasi

0
219

Mkurugenzi wa Idara ya Habari – Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt Hassan Abbasi ametembelea mradi wa ujenzi wa meli ya kisasa ambayo ni meli kubwa kuliko zote katika ukanda wa Afrika Mashariki, pamoja na ujenzi wa Chelezo kwa ajili ya matengenezo na marekebisho ya meli mbalimbali ikiwa ni uwekezaji unaofanywa na Serikali.

Akiwa katika eneo hilo la ujenzi kwenye bandari ya Mwanza Kusini, Dkt Abbasi amesema kuwa ujenzi wa meli mpya ni ahadi iliyodumu kwa zaidi ya miaka 23 iliyopita, ambayo imetekelezwa katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais John Magufuli.

Ameongeza kuwa, ujenzi wa meli mpya itakayokuwa na uwezo wa kubeba abiria 1, 200 umefikia asilimia 33 na utakamilika mapema mwaka 2021, ambapo Serikali imewekeza zaidi ya Shilingi Bilioni 150 kwenye mradi wa meli pamoja na ujenzi wa chelezo.

Aidha, Mkurugenzi huyo wa Idara ya Habari – Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt Hassan Abbasi, ameshuhudia ukarabati unaoendelea katika meli ya MV Victoria, ambayo baada ya kukamilika itasaidia kutoa huduma bora za usafiri kwenye eneo la Ziwa Viktoria.

Amesema kuwa hivi karibuni, Serikali itasaini makubaliano ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa meli katika eneo la Ziwa Tanganyika na uundaji wa meli Tatu mpya na za kisasa katika eneo la Ziwa Nyasa.

Dkt Abbasi ametaja meli zilizokamilika kutokana na utekelezaji wa ahadi za Serikali hadi sasa, kuwa ni meli mbili za mizigo za MV Ruvuma na meli kubwa ya kisasa ya abiria ya MV Mbeya II ambayo tayari imeanza kazi.