Huduma za usafiri kati ya wilaya za Handeni na Kilindi mkoani Tanga zimerejea, baada ya kukamilika kwa ujenzi wa daraja la muda
katika eneo la Nderema.
Ujenzi huo umefanywa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), baada ya daraja la awali kusombwa na maji, kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha mkoani Tanga.
Wasafiri wanaotumia barabara hiyo, wamelazimika kukwama kwa muda wa takribani siku Sita kutokana na kukosekana kwa Mawasiliano baina ya wilaya hizo za Handeni na Kilindi.
Kufuatia kukamilika kwa ujenzi huo, JWTZ imewataka Wakazi wa wilaya za Handeni na Kilindi kulitunza Daraja hilo la Nderema ili liweze kudumu kwa muda mrefu kwa kuwa ni mali yao.
Mkuu wa wilaya ya Handeni, – Godwin Gondwe amelishukuru Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa kuwajengea daraja hilo la muda.
Amesema kuwa, JWTZ imefanya kazi kubwa na kwa muda mfupi, kwa kuwa wamekamilisha kazi hiyo katika kipindi cha siku Moja na Nusu, kazi ambayo ingefanyiwa katika kipindi cha miezi mitatu.