CCM yaridhishwa na mchakato wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa

0
283

Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imekutana leo jijini Dar es salaam, chini ya Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais John Magufuli.
 
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi, -Humphrey Polepole imeeleza kuwa kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ni cha kawaida kwa mujibu wa kalenda ya vikao mwaka 2019 na katiba ya CCM.
 
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kikao hicho pamoja na mambo mengine kimefanya tathmini ya mchakato wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa kuanzia uandikishaji, mchakato ndani ya CCM na maandalizi kuelekea siku ya kupiga kura Novemba 24 mwaka huu.
 
Katika kikao hicho, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM imejiridhisha kuwa mchakato wa Chama wa kuwapata wagombea katika uchaguzi huo wa Serikali za Mitaa umefanyika vizuri.
 
Kamati Kuu imeelekeza katika maeneo ambayo taratibu za uchaguzi hazikufuatwa, taratibu za Kikatiba na za kikanuni ziendelee ili kuhakikisha haki inatendeka, kama ilivyo asili na desturi ya CCM na pale ambapo itathibitika taratibu zilivunjwa kwa hila basi hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa kwa mujibu wa katiba na kanuni zinazoongoza masuala ya uchaguzi, maadili ya viongozi na utumishi katika Chama.
 
Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM pia imefanya uteuzi wa Wanachama Watatu wa CCM wanaoomba kugombea nafasi ya Mstahiki Meya wa jiji la Zanzibar.