Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeahidi kuidhinisha Dola Milioni 455 za Kimarekani ambazo ni zaidi ya Shilingi Trilioni Moja, kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Msalato pamoja na ujenzi wa barabara za mzunguko jijini Dodoma.
Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Dkt Akinwumi Adesina ametoa ahadi hiyo katika ofisi za Makao Makuu ya Benki hiyo zilizopo Abijdan nchini Ivory Coast, wakati wa mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi.
Dkt Akinwumi ameongeza kuwa, AfDB itaendelea kushirikiana na Rais John Magufuli katika kipindi chake cha Uenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) lakini pia kwa Tanzania.
Amesema kuwa, tayari Benki hiyo imeidhinisha Dola Milioni 180 za Kimarekani kwa ajili ya ujenzi wa barabara za mzunguko jijini Dodoma na kwamba kiasi kingine cha Dola Milioni 275 za Kimarekani kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Msalato kinatarajiwa kuidhinishwa mwanzoni mwa mwezi Novemba mwaka huu.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi, ameishukuru Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa ushirikiano inayoutoa kwa Tanzania hasa katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati chini ya Rais John Magufuli.
Amesema kuwa, Benki ya Maendeleo ya Afrika pia iko tayari kufadhili ujenzi wa Reli ya kisasa kipande cha kutoka Isaka hadi Kigali nchini Rwanda na kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo mara baada ya kukamilika kwa mchakato wa utoaji wa fedha hizo.
Waziri Kabudi yuko nchini Ivory Coast kwa ajili kushiriki mkutano wa siku Mbili wa dharura wa Mawaziri wa Fedha uliondaliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika.