Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema kuwa, Serikali inatambua umuhimu wa kuwekeza katika Sekta ya Mawasiliano kama moja ya mkakati wa kuhakikisha azma ya kuwa nchi ya Uchumi wa Kati kupitia Viwanda inafikiwa.
Profesa Ndalichako ametoa kauli hiyo jijini Dodoma, alipomwakilisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika ufunguzi wa Kongamano la Nne la Huduma ya Mtandao Jamii, linalofanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Amesema kuwa, Sekta ya Mawasiliano ni moja ya sekta zinazochangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa Uchumi nchini, hivyo uwekezaji wake ni muhimu.
“Kwa kipindi cha Julai hadi Disemba mwaka 2017, Sekta ya Mawasiliano ilikua kwa asilimia 13.1 na ilikuwa kwenye nafasi ya Pili katika kuchangia ukuaji wa Uchumi nchini,” amesema Profesa Ndalichako.