Ujio wa Miss World nchini wamfurahisha Dkt Mwakyembe

0
2049

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt Harrison Mwakyembe amesema kuwa, ni heshima kubwa kwa Tanzania kutembelewa na Mwenyekiti na Mwendeshaji wa shindano la Mrembo wa Dunia (Miss World) Julia Morley pamoja na Mrembo wa Dunia kwa mwaka 2018 Vanessa Ponce.

Waziri Mwakyembe ametoa kauli hiyo jijini Arusha, wakati wa uzinduzi wa Taulo za kike zinazojulikana kama Uhurupads, uliofanyika katika shule ya Sekondari Moshono.

“Ujio wao hapa Arusha ni heshima kwa Taifa, katika mataifa yote Duniani wameichagua Tanzania, hii ni heshima kubwa na watatuletea zawadi ya Uhurupads ambazo zitawaweka huru watoto wetu katika kutimiza ndoto zao hasa wanapokuwa shuleni” amesema Waziri Mwakyembe.

Kwa upande wake Mwenyekiti na Mwendeshaji wa Shindano la Miss World Julia Morley ameelezea kufurahishwa na jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuwaletea Wananchi maendeleo.

“Nimefurahi sana, Tanzania ni nchi nzuri, nilipopanda ndege kuja hapa nilipata matangazo yanayosisitiza marufuku ya kutumia mifuko ya plastiki, Serikali imefanya vizuri kujali kutunza mazingira”, amesema Morley.