Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama amesema kuwa serikali imefuta baadhi ya ada na tozo zisizoondoa wajibu wa muajiri kulinda afya za wafanyakazi ili kuchochea ujenzi wa uchumi wa viwanda.
Waziri Mhagama ametoa kauli hiyo jijini Dodoma wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari ambapo pamoja na mambo mengine ameelezea mabadiliko mbalimbali yaliyofanywa katika Mamlaka ya Usalama na Afya Mahala Pa Kazi (OSHA) kwa lengo la kutekeleza azma ya serikali ya kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji.
Amesisitiza kuwa lengo la kufuta tozo na ada hizo ni kuboresha mazingira ya biashara, kupunguza gharama za uendeshaji kwa wawekezaji pamoja na waajiri.
“Tumefuta ada mbalimbali ikiwemo ada ya fomu ya usajili ambayo ilikuwa shilingi elfu mbili kwa lengo la kupunguza gharama, tumefuta ada ya usajili wa maeneo ya kazi kwa kuzingatia ukubwa wa eneo ambayo ilikuwa ikitozwa kwa kiasi cha shilingi elfu hamsini hadi shilingi milioni moja na laki Nane kulingana na eneo, hivyo usajili kwa sasa ni bure” amefafanua Waziri Mhagama.
Ameongeza kuwa serikali imefuta ada ya leseni ya kukidhi matakwa ya Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi iliyokuwa ikitozwa shilingi laki mbili kwa mwaka kwa lengo la kuboresha mazingira ya biashara ambapo kwa sasa leseni hiyo itatolewa bure huku tozo ya siku ya ushauri wa kitaalam wa usalama na afya kwa kuzingatia idadi ya wafanyakazi ya shilingi laki Nne na Nusu ikifutwa kwa lengo la kupunguza gharama ili kutoa elimu kwa wahitaji wengi zaidi.
Hata hivyo Waziri Mhagama amesema kuwa OSHA imejikita katika utoaji wa elimu kwa wadau kuhusu takwa la kisheria la kulinda afya za wafanyakazi nchini mahala pa kazi katika kanda mbalimbali na kusimamia mifumo ya utendaji wa watumishi wa mamlaka hiyo ili kuondoa mianya ya rushwa na kukuza uzalendo na uwajibikaji.