Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, ametoa rai kwa Mawaziri wa Mazingira, Maliasili na Utalii wa nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kuwashirikisha Wananchi katika mikakati iliyopo ya kutunza mazingira.
Akifungua mkutano wa Mawaziri wa sekta ya Mazingira, Maliasili na Utalii wa kutoka nchi za SADC unaofanyika jijini Arusha Makamu wa Rais amesema kuwa, Wananchi wanatakiwa kupewa elimu ya kutosha ya namna ya uhifadhi wa mazingira.
Makamu wa Rais pia amewataka Washiriki wote wa mkutano huo kujadili kwa kina na kuweka mikakati ya namna ya kupambana na viumbe vamizi, ambao wamekuwa wakisababisha madhara katika sekta za Kilimo na Uvuvi.
Awali, mkuu wa mkoa wa Arusha, -Mrisho Gambo alitoa wito kwa Washiriki wa mkutano huo wa Mawaziri wa sekta ya Mazingira, Maliasili na Utalii kutoka nchi za SADC kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo mkoani humo.
Mwezi Agosti mwaka huu, Tanzania ilikabidhiwa rasmi Uenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, ambapo kutokea wakati huo mikutano mbalimbali ya kisekta imekuwa ikifanyika hapa nchini.