Kampuni ya Reli ya Russia yakaribishwa kuwekeza Tanzania

0
183

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Reli ya Russia,- Alexander Misharin na kumueleza azma ya Tanzania ya kuimarisha usafiri wa ndani wa reli hasa katika majiji ya Dar es salaam, Mwanza, Dodoma, Arusha, Mbeya na Tanga.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika kwenye mji wa Sochi, Waziri Mkuu Majaliwa ameikaribisha kampuni hiyo ya Reli ya nchini Russia kuwekeza Tanzania hasa katika ujenzi, ufundi na mafunzo ya masuala ya Reli, kwa kuwa kampuni hiyo ina uwezo mkubwa kwenye ujenzi wa reli mpya, ukarabari wa reli, utengenezaji wa injini za treni pamoja na mabehewa ya treni.

“Katika kipindi hiki ambacho Tanzania inajenga reli kwa kiwango cha kisasa pamoja na kufufua reli ya Kaskazini, inaikaribisha Kampuni ya Reli ya Russia kwa mikono miwili ije ifanye mazungumzo rasmi na Wizara husika, pia Serikali ina mkakati wa kujenga reli mpya katika ukanda wa Kusini kutoka Mtwara hadi Ruvuma ili kuiunganisha bandari ya Mtwara na mikoa ya Kusini pamoja na nchi jirani za Malawi na Zambia,”amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Waziri Mkuu amemueleza Misharin kuwa, endapo mazungumzo kati ya Wizara Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na kampuni hiyo yatakuwa na tija na maslahi kwa Watanzania, kampuni hiyo itapewa fursa ya kuwekeza Tanzania.

Waziri Mkuu Majaliwa yuko nchini Russia, kuhudhuria mkutano baina ya Wakuu wa nchi na Serikali kutoka Mataifa ya Afrika na Russia (Russia – Africa Summit), mkutano unaoanza hii leo katika mji wa Sochi.