Guardiola alonga kuhusu Man City

0
806

Kocha wa timu ya Manchester City, Pep Guardiola amesema timu yake
haiwezi kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya msimu huu bila safu yake ya ushambuliaji kuongeza makali kwenye ufungaji wa mabao.

Usiku wa leo, Manchester City watapepetana na timu ya Atalanta ya
Italia kwenye mchezo wa kundi C wa ligi ya mabingwa barani Ulaya huku
wakiwa vinara wa kundi hilo baada ya kushinda michezo yao miwili ya
awali.

Pamoja na kuwa kinara wa kundi lake, Guardiola amesema timu yake
inakosa nafasi nyingi za kufunga mabao hivyo inamuwia vigumu kusema
wanaweza kutwaa taji la Ulaya wakati hawafungi mabao ya kutosha kwenye kila mchezo wanaocheza.

Hata hivyo, Guardiola anaamini wanaweza kubadilika na kuongeza makali
kwenye ufungaji akiongeza kuwa kwa sasa wana kibarua kigumu cha
kuhakikisha wanatwaa kombe hilo lenye hadhi ya juu kwa ngazi ya vilabu
barani Ulaya.

Michezo mingine inayopigwa hii leo kwenye ligi ya mabingwa barani
Ulaya, kwenye kundi hilo la C ni Shakthar Donetk ya Ukraine
wanawaalika Dinamo Zagreb ya Croatia, kwenye kundi A, Club Brugge ya
Ubelgiji itakipiga na PSG ya Ufaransa huku Real Madrid wakiwa wageni
wa Galatasaray ya Uturuki.

Kwenye kundi B, Olimpiacos ya Ugiriki itawaalika Bayern Munich ya
Ujerumani huku Tottenham Hotspur ikiwa mwenyeji wa Crvena Zvezda ya
Serbia na kwenye kundi D, Atletico Madrid itacheza na Bayer Leverkusen
ya Ujerumani na Juventus ya Italia itapambana na Lokomotiv Moscow ya
Russia.