Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani Tanga, Mkuu wa mkoa huo Martine Shigela ameamuru kukamatwa kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa kampuni ya Katani Ltd, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania(TPSF) Salum Shamte.
Shigela ameamuru kukamatwa kwa Shamte kwa tuhuma za ubadhirifu wa zaidi ya Shilingi Bilioni 54.
Mkuu huyo wa mkoa wa Tanga amewaambia Waandishi wa habari kuwa kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni 28 ni fedha za Wakulima wa Mkonge na nyingine ni fedha za Wafanyakazi wa kampuni hiyo ambao ni Wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Shamte na wenzake Wanne wamekamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Tanga, walipokua wakihudhuria kikao chenye lengo la kupokea taarifa ya Tume iliyoundwa na Wizara ya Fedha na Mipango, kuchunguza malalamiko ya Wakulima wa Mkonge dhidi ya kampuni hiyo ya Katani Ltd.