China na Marekani zaendeleza vita ya kibiashara

0
2385

China imesema kuwa italipiza kisasi kwa kutoza ushuru wa dola bilioni sitini za Kimarekani kwa bidhaa za kutoka Marekani, baada ya rais Donald Trump kutangaza kiwango cha ushuru wa ziada kwa bidhaa zinazoingia kutoka China.

China imefikia uamuzi huo baada ya Marekani kutangaza kuwa ushuru wa ziada wa bidhaa kutoka nchini China kuingia nchini humo utakua dola bilioni 200 za Kimarekani.

Mvutano huo ni matokeo ya vita ya kibiashara kati ya China na Marekani, nchi zenye uchumi mkubwa.

Wizara ya Fedha ya China imesema kuwa inalipiza kile ilichokiita ajenda ya Marekani ya kutazama upande mmoja na biashara yenye ushindani usio wa usawa.

Rais Trump ametahadharisha kuwa atalipa kisasi ikiwa wakulima, wafugaji na wafanyakazi wa nchini Marekani watalengwa kwenye uamuzi wa China na kwamba milango ipo wazi endapo China itataka kujadiliana na Marekani kuhusu jambo hilo.

” Tumekuwa na biashara isiyo na uwiano sawa na China, mwaka jana tulipoteza kiasi cha zaidi ya dola bilioni mia tano kwa China, hatuwezi kufanya hivyo” amesema Trump.

Wizara ya mambo ya nje ya China imesisitiza kufanyika kwa mazungumzo kati ya China na Marekani, mazungumzo yenye usawa, kuaminiana na kuheshimiana ikiwa ni njia pekee ya kumaliza mvutano wa kiuchumi na kibiashara kati ya mataifa hayo mawili na kuongeza kuwa kinachofanywa hivi sasa na Marekani hakionyeshi ukweli wala nia njema.