Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo amesema kuwa, idadi ya watu waliojiandikisha kwenye
Daftari la Wapiga Kura kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa imefikia asilimia 68 ya lengo la kuandikisha zaidi ya watu Milioni 22 nchi nzima.
Akitoa tathimini ya uandikishaji huo kwa muda wa siku Saba kuanzia tarehe 8 mpaka 14 mwezi huu, Waziri Jafo amesema kuwa mpaka sasa Wananchi
waliojiandikisha ni zaidi ya Milioni 15 na Laki Tano.
Waziri Jafo ameitaja mikoa Sita iliyofanya vizuri katika siku hizo Saba za uandikishaji kuwa ni Pwani asilimia 80, Dar es salaam asilimia 77, Tanga asilimia 76, Mtwara asilimia 75, Lindi asilimia 75 na Iringa asilimia 74.
Mikoa ambayo haijafanya vizuri katika uandikishaji huo kwa muda wa siku Saba ni Kilimanjaro ambayo iliandikisha kwa asilimia 48, Kigoma asilimia 53 na Arusha asilimia 59.
Awali, zoezi la kuandikisha Wananchi katika Daftari la Wapiga kura kwa ajili ya kushiriki kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 24 mwaka huu lilipangwa kufanyika kuanzia Oktoba Nane hadi 14 mwaka huu.
Hata hivyo Serikali ilitangaza kuongeza siku Tatu za uandikishaji huo kuanzia hii leo, ambapo kwa sasa zoezi hilo litakamilika tarehe 17 mwezi huu.
Waziri Jafo ametoa wito kwa Viongozi wa ngazi zote nchini kuendelea kuwahamasisha Wananchi ili wajitokeze kwa wingi katika siku hizo Tatu za uandikishaji zilizoongezwa.