https://www.youtube.com/watch?v=MtRkkgBOmYw
Rais John Magufuli ameagiza Watumishi wote wa hospitali ya mkoa wa Lindi, – Sokoine kurejesha Shilingi Milioni 49.5 walizojilipa kwa kazi ya kusimamia ujenzi wa wodi ya watoto katika hospitali hiyo.
Akihutubia Wakazi wa Kijiji cha Kiwalala, wakati wa ziara yake mkoani Lindi, Rais Magufuli amesema kuwa katika ukarabati wa hospitali hiyo zaidi ya Shilingi Milioni 86 zimepotea na kati ya hizo zaidi ya Shilingi Milioni 49 wamejilipa baadhi ya Watumishi wa hospitali hiyo.
Rais Magufuli amesema kuwa, Watumishi wote wazirudishe fedha hizo mara moja kwa kuwa kazi waliyofanya haikustahili kulipwa posho.
Rais pia ameshangazwa na hatua ya Mganga Mkuu wa hospitali ya mkoa wa Lindi, – Sokoine kujiuzia gari namba DFPA 6794 likiwa halina tatizo lolote huku hospitali hiyo ikibakia bila gari.
Katika hatua nyingine Rais Magufuli ametangaza rasmi kuwa Halmashauri ya Lindi vijijini inabadilishwa jina na kuwa Halmashauri ya Mtama huku pia akiitangaza tarafa ya Mtama kuwa ndio makao makuu wa Halmashauri hiyo.
