Mwenge wa Uhuru ni alama ya Uzalendo wa Watanzania

0
233

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama amesema kuwa, Mwenge wa Uhuru utaendelea kukimbizwa nchi nzima kwa lengo la kuimarisha Uzalendo na mshikamano wa Tanzania.

Akifungua Kongamano la kumbukumbu ya miaka Ishirini ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mkoani Lindi, Waziri Mhagama amesema kuwa, mbio za Mwenge wa Uhuru zilianzishwa kwa ajili ya kujenga Uzalendo na mshikamano miongoni mwa Watanzania.

Amesisitiza kuwa, Serikali itaendelea kuuenzi mwenge wa Uhuru kutokana na ukweli kuwa unaenzi fikra na maono ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuhusu Uzalendo, mshikamano na amani ya Taifa.

Waziri Mhagama ameongeza kuwa, Mwenge wa Uhuru umekuwa kielelezo cha mshikamano na Uzalendo na umekuwa ukichochea maendeleo kila mahala unapopita katika mikoa na wilaya mbalimbali nchini.