Rais Magufuli aionya mikoa itakayofanya vibaya katika uandikishaji

0
245

Rais John Magufufuli ametoa wito kwa Watanzania kutumia siku Tatu zilizobaki kujiandikisha kwenye Daftari la Wapiga Kura ili waweze kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 24 mwaka huu.

Rais Magufuli ametoa wito huo mjini Mpanda mkoani Katavi wakati akizindua safari ya kwanza ya ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) mkoani humo.

Amesema kuwa tathmini ya awali ya uandikishaji huo inaonyesha baadhi ya mikoa kuzembea katika uhamasishaji kwenye zoezi hilo la uandikishaji, hivyo mikoa hiyo itumie siku zilizobaki kubadilisha hali hiyo.

Rais Magufuli amesema kuwa, anadhani Watanzania hawatamlaumu kwa uamuzi atakaochukua dhidi ya viongozi wa mikoa itakayofanya vibaya katika uandikishaji Wananchi kwenye Daftari la Wapiga Kura mpaka mwisho wa zoezi hilo.

Kwa mujibu wa tathmini ya awali iliyotolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo, mikoa ya Dar es salaam, Kilimanjaro na Arusha haijafanya vizuri katika uandikishaji huo.

Waziri Jafo aliitaja mikoa ya Iringa, Mbeya, Songwe na Tanga kuwa ni miongoni mwa mikoa iliyofanya vizuri katika uandikishaji huo.