Utandikaji reli SGR waanza

0
2165

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe amesema serikali ipo kwenye mpango wa kukamilisha mradi wa chuma wa Liganga na Mchuchuma ili miradi mbalimbali iweze kutumia bidhaa hiyo na kuacha kuagiza chuma kutoka nje ya nchi.

Waziri Kamwelwe ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar Es Salaam baada ya kushuhudia kuanza kwa zoezi la utandikaji reli katika mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa -SGR.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Nchini –TRC, Masanja Kadogosa amesema mataruma ya reli hiyo yanatengenezwa hapa nchini na kuwa ni vyuma vya reli tu ndio vinaagizwa kutoka nje ya nchi.

Meneja mradi katika ujenzi huo Mhandisi Maizo Magedzi amesema reli iliyopo hivi sasa itatandazwa umbali wa kilomita 60 na wakati mzigo mwingine unatarajiwa kuwasili mwezi ujao.

Mradi wa reli ya kisasa utakapokamilika utaweza kubeba tani milioni 17 za mizigo kwa mwaka tofauti na reli iliyopo inayobeba tani milioni tano na kupunguza muda wa safari ambapo treni itakuwa ikitembea kwa spidi ya Kilomita 160 kwa saa.