Rais John Magufuli amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasilino Mhandisi Isack Kamwelwe, kuhakikisha ndege za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) zinaanza safari zake haraka iwezekanavyo mkoani Katavi.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo huko Mpanda mkoani Katavi, wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara na Wakazi wa mkoa huo, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.
Amesema kuwa changamoto zote zilizokua zikisababisha ndege za ATCL kutokwenda mkoani Katavi zimetatuliwa, hivyo kwa sasa hakuna kisingizio chochote.
Ameongeza kuwa, yeye hataondoka mkoani Katavi mpaka ashuhudie ndege ya ATCL imefika mkoani humo.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli, mkoa wa Katavi una vivutio vingi vya utalii, hivyo ni vema ukawepo usafiri wa ndege wa uhakika kwa ajili ya kupeleka Watalii.
