Habinder Seth aandika barua kwa DPP kukiri makosa yake

0
187

Habinder Seth, anayekabiliwa na makosa ya Uhujumu Uchumi amemuandikia barua Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) kukiri makosa yake na kuomba msamaha.

Hayo yameelezwa na Wakili wa Seth, – Michael Ngalo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyopo jijini Dar es salaam mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, – Huruma Shahidi wakati kesi hiyo ilipotajwa.

Seth, ambaye ni Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni ya PAP pamoja na James Rugemalira ambaye ni Mkurugenzi wa VIP, wanakabiliwa na mashtaka 12 wanayodaiwa kuyatenda jijini Dar es salaam na katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India.

Miongoni mwa mashtaka hayo ni kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu , kughushi na kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha na kusababisha hasara ya Mabilioni ya fedha.

Washtakiwa hao walifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Juni 19 mwaka 2017 na hadi sasa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.

Katika maelezo yake, Ngalo ameuomba upande wa mashtaka kuwasaidia kwa kuwa upelelezi wa kesi hiyo umechukua muda mrefu, waelezwe ni lini utakamilika.

Baada ya maelezo ya Ngalo, Wakili wa Serikali, Wankyo Simon ameeleza kuwa wamepokea barua ya Seth, wanaifanyia kazi na majibu yatatolewa.

Kuhusu upelelezi wa kesi hiyo, Wankyo amesema bado haujakamilika na hawezi kuahidi utakamilika lini.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 24 mwaka huu.