Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Watanzania waendelee kushikamana na wazingatie ujumbe wa mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu unaohimiza umuhimu wa maji, uchaguzi wa Serikali za Mitaa, vita dhidi ya rushwa, Malaria, Ukimwi na dawa za kulevya.
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa wito huo mkoani Lindi wakati akizungumza na viongozi wa Halmashauri za Lindi na Ruangwa na Wananchi wa kijiji cha Nangumbu, kwenye uwanja wa shule ya msingi Nangumbu ambako Mwenge wa Uhuru ulipokelewa ukitokea Nyangao.
Ametumia mkutano huo kuwataka Watanzania wote wajiandikishe kwenye Daftari la Wapiga Kura, zoezi lililoanza hapo jana na linalotarajiwa kukamilika tarehe 14 mwezi huu ili waweze kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 24 mwaka huu.
