Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye ameielekeza kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom, kuhamisha mnara wake uliopo katika kijijii cha Bukuku wilayani Nyang’hwale mkoani Geita, ili kumaliza mgororo uliopo baina ya Serikali na Mwananchi anayemiliki eneo ulipojengwa mnara huo na kuujenga kwenye eneo la shule ya Msingi Kulumbai iliyopo karibu na mnara huo ili Wananchi wa kata hiyo waendelee kupata mawasiliano
Mhandisi Nditiye ametoa maelekezo hayo alipofika kwenye kijiji cha Bukuku ulipojengwa mnara huo wakati wa ziara yake wilayani Nyang’hwale na kupatiwa taarifa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Hamim Guyama kuwa mmiliki wa eneo hilo Rukia Kashokelo na mume wake Clement Fungameza wamekataa kusaini mkataba wa Vodacom na wameridhia mnara huo ung’olewe.
“Mnara huu kwa huyu mama uhame tu kwa kuwa upo kwenye jiwe na anataka alipwe Shilingi Milioni Kumi kwa mwaka na anakosesha mawasiliano, amegoma kupokea Shilingi Milioni Mbili na Laki Nne kwa mwaka na eneo hili kuna migodi mitatu na mapato ya takribani Shilingi Bilioni 20 kwa mwaka na ni eneo linalohitaji mawasiliano,” amesema Mhandisi Nditiye.
Ameitaka Kampuni hiyo ya simu ya Vodacom kuhakikisha inahamisha mnara huo ndani ya kipindi cha mwezi mmoja na amepiga marufuku kampuni za simu kujenga minara kwa kutumia ruzuku ya Serikali kwenye eneo la mtu binafsi ili kuepusha migogoro.
Ameelekeza minara hiyo ijengwe kwenye maeneo yanayomilikiwa na Serikali za vijiji, shule, maeneo ya Kanisa ama misikiti ili Wananchi wanufaike na fedha zinazolipwa na kampuni za simu.
Naye Mtendaji wa Kijiji cha Bukuku ulipojengwa mnara huo Eunice Gombanila amemweleza Naibu Waziri huyo wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuwa, mama huyo amekataa kupokea na kusaini mkataba baina yake na Vodacom ambapo alilazimika kukaa na mkataba huo ofisini kwake kwa muda wa wiki nne bila ya mafanikio na alipomfuata alikataa kuusaini na kuridhia ung’olewe.
Vodacom imeishukuru Serikali kwa kutoa maelekezo ya kuhamisha mnara huo na kuahidi kutekeleza maelekezo hayo ili waweze kuendelea kutoa huduma za mawasiliano kwa Wakazi wa kata hiyo.
Ujenzi wa mnara huo umegharimu zaidi ya Shilingi Milioni Mia Mbili.
Akiwa wilayani Nyang’hwale, Mhandisi Nditiye amemwelekeza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL)Waziri Kindamba na Posta Masta Mkuu wa Shirika la Posta kufika wilayani humo mwezi huu na kufungua ofisi zao ili kuweza kuwahudumia Wananchi na kusogeza karibu huduma zao.
