Rais John Magufuli ameiagiza Halmashauri ya mji wa Sumbawanga mkoani Rukwa, kutafuta eneo lingine kwa ajili ya kujenga soko ambalo litatumiwa na Wakazi wa Halmashauri hiyo.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo mkoani Rukwa, wakati akizungumza na Wakazi wa mkoa huo katika uwanja wa Nelson Mandela uliopo mjini Sumbawanga ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.
Amelazimika kutoa agizo hilo baada ya uongozi wa soko lililokuwepo awali kabla ya kuungua moto mwaka 2016 kumueleza kuwa, wanashindwa kufanya shughuli zao kutokana na uongozi wa Halmashauri ya Sumbawanga kuwaeleza kuwa unaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa soko jipya, kubwa na la kisasa.
Rais Magufuli amehoji ni kwa nini fedha zinaendelea kutafutwa mpaka sasa kwa ajili ya ujenzi wa soko hilo la kisasa baada ya lile la zamani kuungua moto, wakati Halmashauri ya Sumbawanga ilikuwa uwezo wa kutenga fedha kila mwaka kutoka kwenye mapato yake kwa ajili ya ujenzi wa soko hilo.
Ameamuru Wafanyabiashara hao waachiwe eneo hilo la zamani ili waendelee na shughuli zao haraka iwezekanavyo na wasihughudhiwe na mtu yoyote, na kuhusu soko hilo jipya, kubwa na la kisasa ameagiza likajengwe kwenye eneo lingine.
Rais Magufuli ameahidi kutafuta Shilingi Milioni Mia Mbili na kuwapatia Wafanyabiashara hao kwa ajili ya kuendeleza eneo hilo la soko la zamani.
