Dkt Bashiru aitembelea TBC

0
2193

Katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt Bashiru Ally amewashauri wafanyakazi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na kuhakikisha wanawaunganisha Watanzania.

Dkt Bashiru ametoa kauli hiyo wakati wa ziara yake ya kwanza  kuifanya TBC akiwa na wadhifa huo ambapo ametembelea vitengo mbalimbali kwa lengo la kujionea utendaji kazi wa vitengo hivyo.

Akiwa TBC, pamoja na mambo mengine, Dkt Bashiru ameelezea kufurahishwa na hazina kubwa ya kumbukumbu katika maktaba ya shirika hilo.

Pia amewahimiza Watanzania wote kuungana badala ya kugawanyika na kuvitaka vyama vya siasa nchini vibadilike ili viondokane na kutawaliwa na wapenda anasa na vyeo.

Kuhusu wanaohamia CCM kutoka vyama vingine, Katibu Mkuu huyo wa CCM amesema kuwa wanavutiwa na utekelezaji wa ilani ya chama hicho kupitia huduma za jamii na mambo mengine mengi mazuri.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dkt Ayoub Rioba amesema kuwa ziara ya Dkt Bashiru TBC ni faraja kwa shirika hilo.

Ameongeza kuwa pamoja na changamoto mbalimbali zilizopo TBC, ni wajibu wa shirika hilo kumulika matatizo ya Watanzania ili yapatiwe ufumbuzi.