Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Singida, – Adili Elinipenda amkamate Afisa Manunuzi wa Chuo cha Ualimu Kinampanda, – Francis Muyombo kwa kukiuka taratibu za manunuzi ya Serikali na kughushi nyaraka.
https://www.youtube.com/watch?v=-ITokmFeoVQ&feature=youtu.be
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo wakati akikagua ukarabati wa majengo ya chuo hicho kilichopo wilayani Iramba, ambapo pamoja na mambo mengine amebaini nyaraka zinazoonesha kuwa kitasa kimoja kimenunuliwa kwa Shilingi Elfu Sabini badala ya Shilingi Elfu Ishirini na Tano.
Baada ya kufanya ukaguzi huo, Waziri Mkuu Majaliwa, pia amemuagiza Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Singida, – Sweetbert Njewike amkamate na kumhoji Joseph Kisaka ambaye alikuwa mzabuni wa chuo hicho kwa kuwapatia vifaa ambavyo ni vya chini ya kiwango.
“Serikali imetoa Shilingi Bilioni 1.4 kwa kila chuo ili kufanya ukarabati wa vyuo vya elimu kikiwemo hiki cha kwenu, ninyi mnanunua vifaa kinyume na utaratibu wa Serikali, hamvikagui, mnaweka tu vitu hafifu ambavyo havidumu, haiwezekani, nyaraka zinaonyesha mlinunua vitasa 368 vya 3-level kwa gharama ya Shilingi 70,000 kila kimoja, lakini vitasa vilivyoko mlangoni ni vya 1-level ambavyo vinauzwa Shilingi 25,000, haya ni mabweni ya Wanafunzi, wanaingi na kutoka kila wakati, ni kwa nini mnaweka vitu cheap wakati mnajua vitaharibika mapema?, maelekezo ya ununuzi wa Serikali yakoje?”, amehoji Waziri Mkuu.
Alipoulizwa wametumia utaratibu gani kununua vifaa hivyo, Mkuu wa Chuo hicho cha Ualimu Kinampanda, – Hamisi Njau alisema kuwa walikuwa wakitumia kamati ya manunuzi ambayo mwenyekiti wake alikuwa ni Makamu Mkuu wa Chuo na Katibu wake ni Afisa Manunuzi, – Francis Muyombo.
