Chalamila apongezwa na Rais Magufuli kwa kuwachapa viboko Wanafunzi

0
337

Rais John Magufuli ampongeza Mkuu wa mkoa wa Mbeya, – Albert Chalamila kwa kuwachapa viboko Wanafunzi 14 wa Kidato cha Tano na Sita katika shule ya Sekondari Kiwanja wilayani Chunya mkoani humo na baadaye kuamuru Wanafunzi 392 wa shule hiyo kurudi nyumbani hadi Oktoba 28 mwaka huu.

Rais Magufuli ametoa pongezi hizo wilayani Mbozi mkoani Songwe, wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara na Wakazi wa wilaya hiyo, akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku Nne mkoani humo.

Amesema kuwa haiwezekani Serikali ikawa inafanya jitihada kubwa za kutafuta fedha kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu, huku watu wengine wakikwamisha jitihada hizo.

Mkuu huyo wa mkoa wa Mbeya alifikia uamuzi wa kuwachapa viboko Wanafunzi hao, baada ya kufika katika shule hiyo ya Sekondari ya Kiwanja akiwa amefuatana na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ya Chunya na kupatiwa taarifa za Wanafunzi 19, wakiwemo Watano wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi kwamba baada ya kukutwa na simu, saa chache baadaye mabweni Mawili ya shule hiyo yaliungua moto.

Chalamila ameamuru Wanafunzi hao walipe Shilingi Laki Mbili kila mmoja kwa ajili ya ukarabati wa mabweni mawili ya shule hiyo yanayodaiwa kuchomwa moto na baadhi yao, fedha ambayo inatakiwa kulipwa Benki.

Kwa Wanafunzi 14 aliowachapa viboko ambao pia walikutwa na simu, watatakiwa kulipa Shilingi Laki Tano na watakaporejea shuleni wanatakiwa kuwa na Wazazi wao.