Wanafunzi 392 wa Shule ya Sekondari Kiwanja waamriwa kurudi nyumbani

0
258

Mkuu wa mkoa wa Mbeya, – Albert Chalamila, ameamuru Wanafunzi 392 wa Kidato cha Tano na Sita katika Shule ya Sekondari Kiwanja wilayani Chunya mkoani humo kurudi nyumbani hadi Oktoba 28 mwaka huu.


Amesema siku watakaporejea shuleni hapo wanatakiwa kuwa na Shilingi Laki Mbili kila mmoja kwa ajili ya ukarabati wa mabweni mawili ya shule hiyo
yanayodaiwa kuchomwa moto na baadhi yao.

Chalamila ametoa uamuzi huo hii leo baada ya kufika katika shule hiyo akiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Mbeya, ikiwa ni siku Moja baada ya kuwachapa viboko Wanafunzi 14 wa shule hiyo kwa madai ya kuchoma moto mabweni ya shule hiyo.

Mkuu huyo wa mkoa wa Mbeya aliwachapa viboko Wanafunzi hao baada ya kufika katika shule hiyo ya Sekondari ya Kiwanja akiwa amefuatana na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ya Chunya na kupatiwa taarifa za Wanafunzi 19, wakiwemo Watano wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi kwamba baada ya kukutwa na simu, saa chache baadaye mabweni Mawili ya shule hiyo yaliungua moto.

Amesisitiza kuwa, Wanafunzi ambao hawatatekeleza amri ya kulipa fedha kupitia Benki na kutofika shuleni Oktoba 28 mwaka huu, watafuatwa na pingu majumbani mwao na hawataruhusiwa kufanya mtihani wao wa mwisho.

Kwa mujibu wa Chalamila, Wanafunzi 14 aliowachapa viboko ambao pia walikutwa na simu, watatakiwa kulipa Shilingi Laki Tano na watakaporejea shuleni wanatakiwa kuwa na Wazazi wao.

Ameongeza kuwa, fedha hizo zinatakiwa kulipwa Benki kabla ya tarehe 18 mwezi huu na Wanafunzi wapeleke risiti za malipo shuleni.