DPP awaonya Mawakili walaghai

0
159

Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) Biswalo Mganga ametoa onyo kwa baadhi ya Mawakili kuacha mara moja kuwalaghai Watuhumiwa wa makosa ya Uhujumu Uchumi waliokiri kutenda vitendo hivyo kwa kuwashawishi kutoa fedha kwa madai ya kwenda kuzilipa kwenye Ofisi ya DPP.

Akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dar es salaam, DPP Mganga amesema kuwa, amelazimika kutoa onyo hilo baada ya kuwepo kwa taarifa kuwa baadhi ya Mawakili wamekua wakichukua fedha kwa Watuhumiwa kwa madai ya kuzifikisha katika Ofisi ya DPP, lakini hawazifikishi.

Amesema kuwa, kufuatia hali hiyo, Serikali imefungua akaunti maalum katika Benki Kuu ya Tanzania (BOT ) ili watuhumiwa hao wa Uhujumu Uchumi waliokiri kutenda vitendo hivyo na kuomba msamaha waweze kuweka fedha hizo.

Amesisitiza kuwa, mtuhumiwa yoyote atakayeweka fedha kwenye akaunti tofauti na akaunti hiyo ya Serikali hatahesabika kuwa amelipa fedha hizo.

Aidha Mkurugenzi huyo wa Mashtaka Nchini amesema kuwa, Ofisi yake haitasita kuwachukulia hatua Mawakili wote wawe wa Serikali ama Binafsi watakaobainika kujihusisha na ulaghai huo.

Septemba 22 mwaka huu, Rais John Magufuli alitangaza msamaha  kwa Watuhumiwa wa makosa ya Uhujumu Uchumi ambao wataandika barua za kukiri makosa, kuomba radhi na kukubali kulipa fedha walizozipata kinyume cha sheria, ambapo tayari Ofisi ya DPP imetangaza kupokea barua 467, huku jumla ya Shilingi Bilioni 107 zimeisharejeshwa.