Tanzania yapiga hatua katika usambazaji wa maji safi

0
175

Tanzania imepiga hatua katika usambazaji wa huduma ya maji safi na salama Mijini kutoka asilimia 45 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 95 mwaka huu,   na asilimia 46 mwaka 2015 hadi asilimia 65 mwaka huu kwa upande wa vijijini.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt Hassan Abbasi wakati akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es salaam, ikiwa ni mkutano wake wa kawaida wa kila mwezi wenye lengo la kuelezea utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali.

Amesema kuwa,  mwaka 2015 Serikali iliweka lengo la kufikisha maji vijijini kwa asilimia 85 na mijini asilimia 95 ifikapo mwaka 2020, na kwamba katika kufikia lengo hilo kazi kubwa imefanyika ambapo zaidi ya miradi 289 na vituo zaidi ya 89,780 vimekamilika kwa gharama ya zaidi ya Shilingi Bilioni 336.15.

“Kazi kubwa inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali vijijini ikiwemo kukamilisha vituo 44,590 vya maji”, amesema Dkt Abbasi.

Dkt Abbasi ametumia mkutano huo, kuwaondoa hofu Wakulima wa zao la Korosho kufuatia kauli za baadhi ya watu kuwa msimu mpya wa korosho unakuja, na hivyo watakosa maghala ya kuhifadhi korosho zao, jambo ambalo amesema haliwezekani.

Amefafanua kuwa hadi sasa, zaidi ya Tani 98,860 zimekwishachukuliwa na kusafirishwa nje ya nchi kupitia Bandari za Mtwara na Dar es salaam ambazo ni sawa na asilimia 41 ya korosho zote, na zoezi la kuondoa korosho zilizobaki kupelekwa kwa Wanunuzi linatarajiwa kukamilika Oktoba 21 mwaka huu.

“Naomba kusisitiza tena, faida kubwa ya mchakato huu ni kwa wakulima kupata bei ya haki katika zao la korosho, lakini funzo la korosho si tu limeweka mazingira mazuri zaidi katika misimu ijayo ambapo  korosho itanunuliwa kwa mfumo madhubuti lakini pia mazao mengine yamepata nguvu ya kuwekewa mifumo na hivyo wakulima kupata bei inayowanufaisha kwa kuwapa faida”, amesema Dkt Abbasi.