Waziri Mkuu akagua ujenzi wa hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini

0
220

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Wananchi wanaoishi pembezoni mwa ujenzi wa Hospitali ya Kanda ya Kusini kuhakikisha wanakuwa walinzi wa vifaa vinavyotumika kwa ajili ya ujenzi huo.

Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa hospitali hiyo inayojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kama Mkandarasi katika eneo la Mitengo kwenye Manispaa ya Mtwara -Mikindani.

Shilingi Bilioni 15.8 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi huo na tayari NHC imeshalipwa Shilingi Bilioni 6.3 kwa ajili ya ujenzi huo ambao utakamilika katika kipindi cha mwaka mmoja ujao.

Akihutubia Wakazi wa eneo hilo, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa hospitali hiyo kutapunguza gharama za Wananchi wa Kanda ya Kusini na nchi jirani, za kusafiri kufuata matibabu kwenye hospitali zingine za Rufaa.

Ametoa wito kwa Wadau mbalimbali kushirikiana na Shirika la Nyumba la Taifa ili liweze kukamilisha mradi huo muhimu na kwa wakati.

Aidha Waziri Mkuu amesema kuwa, miradi mbalimbali ya kimkakati inayotekelezwa nchini imelenga kutoa huduma bora kwa Wananchi na kutoa fursa ya ajira kwa Wazawa katika maeneo inapotekelezwa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa Dkt Maulid Banyani amemuahidi Waziri Mkuu Majaliwa kuwa, Shirika hilo litakamilisha ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini kwa wakati.

“Ninaahidi mbele yako Mheshimiwa Waziri Mkuu kuwa, lengo letu ni kufanya kazi hii usiku na mchana ili kuikabidhi hospitali hii kabla ya mwezi Agosti mwaka 2020 ili iweze kutoa huduma kwa wana Kusini na Watanzania wote ambao watakuwa na matatizo ya kiafya”, amesema Dkt Banyani.