Serikali kuendelea kuwalinda Wazee

0
144

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa, Serikali itaendelea kuwalinda Wazee dhidi ya vitendo vya ukatili na kuwawekea miundombinu pamoja na mazingira bora katika kutumia vyombo vya usafiri.
 
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo hii leo, wakati akihutubia Wananchi katika kilele cha Maadhimisho ya Siku Wazee Duniani yaliyofanyika Kitaifa kwenye uwanja Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.

Amezitaka Taasisi zinazotoa huduma kwa Wazee, kutoa huduma stahiki na kuepuka kutumia fedha nyingi kwenye mikutano, warsha na makongamano ambayo hayawafaidishi Wazee wenye uhitaji.
 
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, utoaji huduma kwa Wazee ni moja ya vipaumbele vya Serikali na kwamba itaendelea  kuchukua hatua za makusudi kwa lengo la kuboresha hali na maisha ya Wazee nchini.

Ameongeza kuwa, Serikali inaendelea kutekeleza Sera ya Taifa ya Afya ya mwaka 2007 ambayo inatambua kuwa Wazee ni kundi maalumu linalohitaji kupewa kipaumbele katika kupata huduma bora za afya, inaweka mkazo kuwa Wazee wote wenye umri wa miaka Sitini na kuendelea na wasiokuwa na uwezo watibiwe bila malipo. 
 
Hata hivyo, Waziri Mkuu Majaliwa ameendelea kuziagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha zoezi la kuwatambua na kuwapatia vitambulisho Wazee wasiokuwa na uwezo linakuwa endelevu ili waweze kunufaika na huduma ya matibabu bila malipo  pindi wanapougua. 
 
Awali,Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,- Ummy Mwalimu alieleza kuwa lengo la maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani ni kuongeza uelewa wa jamii kuhusu masuala mbalimbali ya Wazee ikiwa ni pamoja na kutafakari fursa za changamoto zinazowakabili na namna ya kuzitatua.

Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 ilionyesha kuwa, Tanzania inakadiriwa kuwa na Wazee zaidi ya Milioni Mbili na Nusu ambao ni sawa na asilimia 5.6 ya Watanzania wote.