Waziri Mkuu ahoji utendaji kazi wa Mkuu wa wilaya wa Kilolo

0
346

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa mkoa wa Iringa, -Ally Happi kufuatilia utendaji kazi kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya ya Kilolo, kufuatia Watumishi 14 wa ofisi hiyo wakiwemo madereva Kumi kuhamishwa baada ya mkuu wa wilaya hiyo Asia Abdallah kudai kuwa hawafanyi kazi ipasavyo.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo, wakati akizungumza na Watumishi wa wilaya ya Kilolo, halmashauri ya wilaya ya Kilolo pamoja na Madiwani wa halmashauri hiyo, akiwa katika siku ya Nne ya ziara yake ya kikazi mkoani Iringa.

Amesema kuwa, ni muhimu kwa Viongozi wakatambua dhamana zao katika utekelezaji wa shughuli zao pamoja na kuwatambua, kuwajali na kuwathamini Watumishi wa kada zote wakiwemo madereva, na kuwapa maelekezo kwa wakati kwa kuwa nao ni Binadamu na Wanafamilia.

Amemtaka Mkuu huyo wa wilaya ya Kilolo,-Asia Abdallah ahakikishe anashirikiana vizuri na Watumishi wengine kwa kuwa watumishi wengi wamehamishwa tangu aingie katika ofisi hiyo na hata wanaoletwa wanalalamika na wanaomba wahamishwe.

Amesema kuwa, Mkuu huyo wa wilaya anawaona Watumishi wengine katika ofisi hiyo hawana uwezo wakiwemo Wasaidizi wake kama madereva, watunza kumbukumbu na Makatibu Muhtasi.

“Hata aliyekuwa Katibu Tawala wa wilaya hii alihamishwa kwa sababu za kutoelewana na DC, na hata huyu Katibu Tawala wa wilaya aliyepo sasa hana raha anataka kuhama kwa sababu hizo hizo, lazima tuwatambue wasaidizi wetu na majukumu yao, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya haiwezekani ikawa hivi, lazima kuna shida kuwaondoa watumishi wote, Mkuu wa Mkoa fuatilia hii ni mpya, hapa tunataka tujue DC wako anataka dereva wa aina gani, tangu amefika hapa madereva 10 wote hawafai?”, amehoji Waziri Mkuu Majaliwa.