Askari waliojeruhiwa katika ajali wahamishiwa Muhimbili

0
310

Askari 11 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kati ya Ishirini waliojeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea jana kwenye eneo la mpaka wa wilaya ya Tanganyika na Katavi, wamehamishiwa hospitali ya Taifa Muhimbili iliyopo jijini Dar es salaam kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.

Majeruhi hao ambao mara baada ya ajali hiyo walikuwa wakipatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Kigoma, – Maweni, wamesafirishwa kutoka mkoani Kigoma Alfajiri ya leo kwa ndege ya JWTZ.

Majeruhi wengine Tisa wa ajali hiyo wameruhusiwa kutoka hospitalini baada ya kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo ya Rufaa ya mkoa wa Kigoma.

Askari hao walijeruhiwa baada ya lori la Jeshi walilokua wakisafiria kwenda mkoani Katavi kutekeleza majukumu mbalimbali, kuacha njia na kugonga mti katika eneo lenye kona, na kisha kuanguka.

Katika ajali hiyo, Askari wawili wa JWTZ kikosi cha 24KJ mkoani Kigoma walifariki Dunia.