Wabunge Uingereza sasa kuanza kazi

0
1252

Wabunge nchini Uingereza wanaelekea kazini, baada ya Mahakama Kuu n chini humo kutoa uamuzi kuwa, haikuwa haki kwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo Borris Johnson kuahirisha Bunge hadi mwezi Oktoba mwaka huu.

Johnson alitangaza kuwa, Bunge la nchi hiyo limeahirishwa hadi katikati ya mwezi Oktoba, ambapo zitakuwa zimebakia siku Kumi na Tano tu kabla ya nchi hiyo kujitoa rasmi kwenye Umoja wa nchi za Ulaya.

Uamuzi huo ulipingwa na Wabunge wengi wa Uingereza, ambao walisema kuwa huo ni muda mfupi kwao kuchangia muswada kuhusu hatua ya nchi yao kujitoa kwenye Umoja wa nchi za Ulaya.

Mahakama Kuu ya Uingereza imesema kuwa hatua hiyo ni uvunjaji wa sheria za nchi hiyo.

Johnson muda mfupi uliopita amerejea jijini London akitokea nchini Marekani, ambapo amelazimika kusitisha kuhudhuria mkutano wa Umoja wa Mataifa unaofanyika mjini New York, baada ya uamuzi huo wa Mahakama.